Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi
wa Iraq Kanda ya Afrika ya Mashariki Dr. Adel Mustafa Kamil ofisini
kwake vuga Mjini Zanzibar. Katikati ni Mkalimali wa mazungumzo ya Viongozi hao Sheikh Nauman Jongo kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar.
*********************************
Serikali
ya Iraq inafikiria wazo la kuanzisha chuo cha mafunzo ya Taaluma ya
uchimbaji wa mafuta na gesi ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika azma yake ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Balozi wa Iraq katika kanda ya Afrika Mashariki Dr.
Adel Mustafa Kamil ambaye makao makuu yake yapo Mjini Nairobi Nchini
Kenya alisema Iraq imeamua kufungua ukurasa mpya wa mawasiliano na
marafiki zake ikilenga zaidi mataifa ya Bara la Afrika.
Akizungumza
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini
kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar Balozi wa Iraq katika Kanda ya Afrika
Mashariki Dr. Adel Mustafa alisema hatua hiyo itaweza kuijengea Uwezo
Tanzania ambayo tayari imeshaonyesha dalili za kuwa na rasilmali hiyo.
Alisema wakati Tanzania inajiandaa kuwa na muelekeo wa uchumi mpya ni vyema mipango hiyo ikaenda sambamba na upatikanaji wa wana taaluma wazalendo watakaokuwa na uwezo kamili wa kuendesha miradi hiyo kitaalamu.
Hata
hivyo Balozi Adel Mustafa alishauri kwamba itapendeza zaidi iwapo
baadhi ya wanafunzi hao wakapatiwa mafunzo ya mwanzo Nchini Iraq ili
kupata taaluma ya nadharia na ile ya vitendo.
Balozi huyo wa Iraq Kanda ya Afrika ya Mashariki Dr. Adel Mustafa alifahamisha kwamba Iraq imepita katika kipindi kizito cha vita kilichopelekea kulega lega kwa uhusiano wake na Mataifa mengi Duniani.
Dr.
Adel Mustafa alisema hatua inayoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Iraq
hivi sasa ni kuwatumia Viongozi na maafisa wake kuhakikisha uhusiano
wake na nchi rafiki unarejea kama kawaida.
Katika
kuendelea kudumisha uhusiano wa pande hizo mbili Balozi Adel Mustafa
ametoa ombi maalum kwa Viongozi wa Juu wa Serikali zote mbili ile ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya
ziara maalum Nchini Iraq kwa lengo la kudumisha uhusiano huo.
“ Tunaanza kufarajika hatua kwa hatua kufuatia maombi tunayopokea kutoka kwa mataifa yanayohitaji watendaji na wananchi wao kupatiwa fursa za masomo Nchini Iraq “. Alifafanua Dr. Adel Mustafa Kamil.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alimueleza Balozi wa Iraq Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Dr. Adel
Mustafa Tanzania imefarajika kuona Iraq imerejea tena katika hali ya
utulivu na amani.
Balozi
Seif alisema migogoro ya kisiasa inayotokea au kubuniwa na baadhi ya
watu wakorofi popote pale duniani mara nyingi husababisha kuwakosesha haki zao wananchi walio wengi.
Alieleza
kwamba amani ni muhimu na bila ya hilo hakuna maendeleo. Hivyo wananchi
wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla wanatarajia kwamba amani waliyonayo
Wairaq itawapa fursa ya kupiga hatua zaidi katika kuimarisha uchumi
wake.
“ Tanzania ilishtuka kidogo kutokana na mitihani iliyoipata nchi ya Iraq. Lakini hivi
sasa tumefarajika kusikia na wakati mwengine kuona katika mitandao
kwamba Iraq imerejea katika hali ya amani kama kawaida yake “.
Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimfahamisha Balozi huyo kwamba Zanzibar inahitaji zaidi kupata fursa za taaluma katika kuwaendeleza wananchi wake hasa katika sekta ya mafuta na Gesi.
Balozi Seif alisema Taifa la tayari limekuwa na uzoefu na kupiga hatua kubwa katika taaluma ya masuala ya mafuta na gesi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/4/2013.
No comments:
Post a Comment