Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na ndugu wa marehemu Meja JeneraliMstaafu Makame Rashidi Mnalihinga baada ya kulazwa katika hospitali yaLugalo na kufariki katika hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi ya shinikizo la damu jana. Rais alikwenda kuwafariji wafiwa nyumbani kwake Mikocheni, ambapo marehemu atasafirishwa Jumanne kwenda Mtwara kwa maziko. Kulia ni mtoto mkubwa  wa marehemu, Kwame Makame pamoja. (Picha na Robert Okanda).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashidi, ambaye ameaga dunia alfajiri ya Jumapili, Aprili 14, 2013 katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar Es Salaam.
Enzi za uhai wake, mbali na kuwa mkuu wa JKT, Meja Jenerali Makame pia alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Balozi wa Tanzania katika Malawi.
Kufuatia msiba huo, Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kuomboleza kifo hicho.
Rais Kikwete ameeleza kuwa alimfahamu Jenerali Makame enzi za uhai wake kwa miaka mingi katika utumishi wa umma. Alimfahamu kama mtumishi mtiifu na msikivu ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kama kiongozi mwadilifu na mwaminifu katika nafasi yake ya Ukuu wa Mkoa na kama Mwanadiplomasia mahiri ambaye aliiwakilisha Tanzania nje ya nchi kwa uhodari mkubwa.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashid ambaye nimejulishwa kuwa ameaga dunia asubuhi ya leo kwenye Hospitali ya Lugalo. Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Nakuomba kupitia kwako vile vile unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa maofisa wote wa Jeshi letu ambao wameondokewa na ofisa mwenzao na askari wote ambao wameondokewa na kiongozi wao. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia ya Marehemu Makame Rashid pole nyingi kwa msiba huu mkubwa wa kuondokewa na mhimili wa familia.”
“Nakuomba uwajulishe kuwa niko nao katika msiba huo mkubwa kwa sababu naelewa huzuni na machungu yao katika kipindi hiki kigumu. Nawaombea subira za Mwenyezi Mungu awavushe katika kipindi hiki. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenye Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Makame Rashid. Amina”
-Wakati huo huo, Rais kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete asubuhi ya jana, jumapili tarehe 14 Aprili, 2013 amekwenda kuwajulia hali wafiwa nyumbani kwa Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashid eneo la Mikocheni, mjini Dar Es salaam.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.