Balozi Leslie Rowe kutoka ofisi ya Serikali ya Marekani anayeshughulikia mambo ya afya.(Picha na Maktaba).
Na Anna Nkinda – Maelezo
Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa dharula wa kupunguza makali ya VVU na Ukimwi (PEPFAR) imeipatia Serikali ya Tanzania dola za kimarekani millioni tatu fedha ambazo zitatumika kuwapima na kuwatibu wanawake wanaosumbuliwa na matatizo ya saratani ya mfuko wa kizazi.
Hayo yamesemwa jana na Balozi Leslie Rowe kutoka ofisi ya Serikali ya Marekani anayeshughulikia mambo ya afya wakati akiongea na watu mbalimbali walioshiriki mkutano wa wake wa Marais wa Afrika uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Aidha Serikali ya Marekani pia imetoa mashine 16 za cryotherapy ambazo zitatumika kama sehemu ya matibabu kwa ugonjwa wa saratani ya mfuko wa kizazi katika Hospitali ya Kansa ya Ocean Road.
Balozi Rowe alisema kuwa upatikanaji na mashine hizo utawasaidia wanawake wengi ambao wanasumbuliwa na ugonjwa wa Kansa ya shingo ya kizazi kuweza kupata huduma ya vipimo na matibabu mapema na haraka.
“Kutokana na maambukizi ya VVU wanawake wengi wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwa kushirikiana na PEPFAR tutaendelea kuwaunga mkono utepe wa pink,utepe mwekundu kuokoa maisha ya wanawake.
Jitihada za pamoja zinahitajika kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii na kuimarisha miundombinu ili kuhakikisha kuwa tunatoa vipimo na matibabu ya saratani kwa wakati”, alisema Balozi Rowe.
Akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Mama Kikwete aliishukuru Taasisi ya Bush kwa kufanya mkutano huo nchini na kusema kuwa mambo yaliyojadiliwa ni upatikanaji wa elimu kwa mwanamke, upatikanaji wa Afya bora na kumuwezesha mwanamke kiuchumi.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa mwanamke ni mtu muhimu sana katika jamii haijalishi ana elimu kiasi gani yeye ni mlezi wa familia na ukimwezesha mwanamke kielimu ni ukombozi mkubwa katika jamii kwani ni rahisi kwake kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.
“Miaka ya nyuma kutokana na baadhi ya watu kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa wa Ukimwi waliweza kuamini kuwa mtu akiwa na maambukizi ya ya VVU amerogwa lakini hivi sasa baada ya watu kupata elimu wkamekuwa na uelewa mkubwa.
“Ukimwezesha mwanamke kielimu na kiuchumi anakuwa na uhuru wa kufanya mambo yake bila ya kutegemea msaada kutoka kwa mme wake ninachowaomba wanawake wenzangu mfanye kazi kwa bidii kwani mwanamke akiwa na kipato cha kutosha hawezi kudharaulika”, alisema Mama Kikwete.
Alisema kuwa zamani wanawake wasiokuwa na kazi walikuwa wanaitwa magoli kipa ingawa walikuwa na kazi kubwa ya kuangalia familia na jamii ikasahau kuwa wanawake ndiyo wazalishaji mali. Pia aliwaomba wanawake wasiogope kuchangamkia fursa zinazopatikana na wasiache kumuunga mkono mwenzao pale anapoomba nafasi ya kupata fursa hizi kwani wakiwa pamoja wanaweza.
Katika mkutano huo pia Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa Marekani George Bush walitambulisha rasmi Utepe wa Pinki , Utepe mwekundu ambayo ni alliance inayofanya kazi ya kupambana na kansa ya saratani ya mfuko wa kizazi na saratani ya matiti katika nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara na Amerika ya Kusini.
Tanzania ni nchi ya tatu Barani Afrika kutambulisha Utepe wa Pinki , Utepe mwekundu alliance nchi zingine ni Zambia na Botswana.
Mkutano huo wa siku mbili uliomalizika jana uliandaliwa na Taasisi ya Rais mstaafu wa Marekani George Bush na kuhudhuriwa na baadhi ya wake Wa Marais wa Afrika na Mke wa Waziri mkuu mstaafu Wa Uingereza Cherie Blair.
No comments:
Post a Comment