Mtambo wa kusafishia gesi Mnazi Bay, Mtwara. |
Rais Jakaya Kikwete ametaka uchimbaji gesi asilia uharakishwe ili kuongeza kasi ya kuondoa umasikini kwa wananchi.
Aidha alisisitiza kuwa jukumu kubwa la gesi asilia nyingi iliyogunduliwa na inayoendelea kugunduliwa nchini ni kuwatoa Watanzania katika umasikini.
“Maandalizi ya uchimbaji yasichukue muda mrefu … miaka 10 hivi… huu ni muda mrefu sana, kwa sababu wananchi wetu wanahitaji kuona manufaa ya gesi asilia katika kipindi kifupi iwezekanavyo”.
Aidha, Rais amesema ni lazima wananchi waone na kuthibitisha manufaa ya gesi hiyo kwa maendeleo yao katika kipindi kifupi.
Ameongeza kuwa uchochezi wa baadhi ya wanasiasa kuhusu gesi asilia iliyogunduliwa nchini ni changamoto ambayo, hata hivyo, Serikali yake iko tayari kupambana nayo.
Alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kundi la Kampuni za British Gas (BG) Chris Finlayson, moja ya kampuni ambazo zimegundua gesi na kuanza kuwekeza katika uchimbaji rasilimali hiyo muhimu.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais alimwambia Finlayson na ujumbe wake, kuwa gesi asilia inayoendelea kugunduliwa nchini ni raslimali muhimu na lazima itumike katika “kuwatoa watu wetu katika umasikini na lazima ibadilishe maisha yao.”
Alisema: “Ni dhahiri kuwa nyie wabia wetu mtanufaika na gesi asilia kutokana na uwekezaji wenu, lakini kimsingi tunataka gesi hii inufaishe watu wetu, iwatoe katika umasikini. Kama gesi hiyo inaweza kutuingizia pato la dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka, ni dhahiri tunaweza kuibadilisha nchi hii ikawa mbingu.”
Kuhusu wanasiasa wachochezi ambao wamekuwa wanachochea wananchi wa Mtwara kudai gesi isitoke mkoani humo na kuwa itumike kwa manufaa yao pekee, Rais Kikwete alisema:
“Uchochezi wa wanasiasa ni changamoto. Hakuna shaka. Lakini hii ni changamoto ambayo Serikali itapambana nayo na ina uwezo wa kutosha wa kumaliza changamoto hiyo.”
Finlayson alimweleza Rais maendeleo ya maandalizi ya uchimbaji wa gesi asilia hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa kitanzania kusomea utaalamu wa gesi hiyo.
No comments:
Post a Comment