Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za usafiri ya China (CITS) Zou Wang Sheng (mwenye fulana nyekudu) kushoto ya Sheng ni Balozi mdogo wa China Madam Chen huko Ofisini kwake Kikwajuni Mjini Zanzibar.Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za usafiri ya China (CITS) Zou Wang Sheng baada ya mazungumzo yao huko Ofisini kwake Kikwajuni Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
………………….
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Kuokosekana kwa Matangazo ya Vivutio vya Zanzibar nchini China kumetajwa kuwa sababu inayopelekea Watalii wanaotoka nchini huko kushindwa kuja Zanzibar kufanya shughuli za Utalii.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za usafiri ya China (CITS) Zou Wang Sheng ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk huko Ofisini kwake Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Sheng amesema China ni miongoni mwa nchi zinazotoa Wataii wengi kutembelea nchi tofauti duniani lakini Wachina walio wengi hushindwa kuja Zanzibar kutokana na kukosa taarifa zinazohusu vivutio hivyo.
Amedai kuwa hata katika Balozi ya Tanzania nchini China hakuna Matangazo yanayohusu vivutio vya Zanzibar badala yake kunapatikana Matangazo ya Mbuga za Serengeti na Manyara ambazo zote ziko Tanzania Bara.
Sheng ambaye ni mara yake ya kwanza kuja Zanzibar ameongeza kuwa kutokana na mazigira mazuri yakitalii yaliyopo Zanzibar anaamini kama kutafanywa mkakati thabiti wa kuvitangaza Vivutio vya Zanzibar hapana shaka zaidi ya Watalii 200,000 wanaweza kuitembelea Zanzibar kwa mwaka.
Ameelezea kuvutiwa kwao na Fukwe, hali ya hewa na mazingira ya Zanzibar kwa ujumla wake na kuahidi atakaporudi atafanya kazi ya kushawishi makundi ya Wageni kuja kujionea vivutio hivyo.
“Tumetembea nchi nyingi dunia kufanya ziara za kitalii lakini ukweli nikwamba ni nchi chache sana za visiwa duniani zenye vivutio vizuri kama Zanzibar ” Alisema Sheng
Awali Waziri wa habari Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema Zanzibar na China zimekuwa na mashirikiano makubwa kwa muda mrefu hasa katika sekta za elimu, Afya na teknolojia na kwamba kwa sasa Sekta ya Utalii inapaswa kupewa mkazo wa pekee.
Ameongeza kuwa Zanzibar imekuwa ikipokea Watalii kutoka nchi nyingi za Ulaya na hasa Wataliano na kwamba umefika muda sasa walau Theluthi ya Watalii kutoka China kuja kutembelea Zanzibar.
“Taarifa zinaonesha China inatoa Watalii zaidi ya Milioni moja kwenda kutembelea nchi tofauti duniani sasa tunataka walau watalii laki tatu watembelee Zanzibar kwa mwaka ” Ameongeza Waziri Mbarouk.
Ameongeza kuwa mazingira ya Zanzibar ni mazuri kwa vivutio vingi vya utalii na hali ya kisiasa ilivyotengamaa na kulitaka Shirika hilo kufanya jitihada zake ili kuwepo kwa Safari za ndege zinazotoka China na kuja Zanzibar.
Waziri Mbarouk amewahakikishia Wawekezaji hao kila aina ya ushirikiano ili kuona Sekta ya Utalii nchini inasonga mbele kupitia Watalii wa kichina.
Kwa upande wake Balozi mdogo wa China nchini Madam Chen Queman amesema kuwa walipokea ushauri kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Menyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kusaidia kuitangaza Zanzibar ambapo ujio wa kampuni hiyo ni utekelezaji wa shauri hilo.
Ameongeza kuwa njia pekee ya kufikia malengo yaliyokusudiwa ni kuhakikisha kunakuwepo mawasiliano na mashirikiano ya moja kwa moja kati ya Kampuni hiyo na Mamlaka ya Ukuzaji Vitegauchumi Zanzibar ZIPA.
Madam Chen amesema ZIPA ndio watakao kuwa Wenyeji wa Kampuni hiyo ili kujua nini kifanyike katika hatua za mwanzo kuhakikisha Zanzibar inafaidika na Watalii kutoka nchi ya China.
No comments:
Post a Comment