Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyeshika mkasi) akikata utepe kuzindua rasmi
ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo. Kushoto kwa Rais ni Waziri wa Ujenzi
Mhe. Dkt. John P. Magufuli na kulia kwa Rais ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi
Alhaj Eng. Mussa Iyombe. Wengine katika picha ni baadhi ya Mawaziri, Wabunge na
Viongozi wa Mikoa ya Geita na Kagera walioshiriki katika sherehe hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga –
Biharamulo.
Lori aina ya Scania la Kampuni ya MAP CO Ltd.
likiwa na usajili namba T 895 AFH/T 226 AGB kama lilivyokutwa eneo la
Manyoni mkoani Singida likiwa limekatika katikati kutokana na kuelemewa na uzito
wa mzigo lililoubeba.
-----------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete amemtaka Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli
kuhakikisha kuwa Sheria ya Usalama Barabarani inasimamiwa vizuri ili
kuhakikisha kuwa barabara zinazojengwa nchini zinadumu kwa muda uliokusudiwa.
Akizungumza katika eneo la Buziku mkoani Geita wakati akizindua
ujenzi wa barabara ya Bwanga hadi Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67, Rais
Kikwete alisema kuwa wizara ya Ujenzi ni lazima ihakikishe inasimamia sheria
zilizopo na hasa hii ya kutoruhusu magari yenye uzito uliozidi viwango
vilivyoainishwa katika Sheria Namba 30 ya Mwaka 1973.
Akisistiza umuhimu wa kutunza barabara Rais Kikwete alibainisha
kuwa “adui wakuu watatu wanao sababisha barabara kuharibika mapema ni; magari
yanayobeba mizigo zaidi ya uzito uliowekwa kisheria, ujenzi duni usiozingatia
viwango na kuachwa kwa maji kuzagaa barabarani”.
Wakati huo huo Rais Kikwete alielezea kufurahishwa kwa kuanza
ujenzi wa mradi huo kwani wapo baadhi ya watu waliokuwa waliokuwa wakieneza
taarifa kuwa sehemu hiyo ya barabara haiwezi kujengwa lakini sasa wameumbuka.
Awali akitoa maelezo ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa Tanroads
Injinia Patrick Mfugale alielezea kuwa mradi mradi wa ujenzi wa barabara hiyo
kwa kiwango cha lami umegharimu Shilingi bilioni 55 fedha zote zikiwa
zimetolewa na Serikali ya Tanzania. “Mradi huu utajengwa kwa muda wa miezi 27
na hivyo kukamilika mwezi Februari mwaka 2015” alisema Injinia Mfugale.
Naye Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Magufuli alimhakikishia Rais
Kikwete kuwa wizara yake itahakikisha kuwa inamsimamia mjenzi wa mradi huo
ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Ltd. ya kutoka Jamhuri ya Watu wa China ili
aukamilishe kwa muda na viwango vilivyokusudiwa na bila ya visingizio vya
nyongeza ya gharama.
Akimpongeza Rais kwa kutekeleza ahadi yake, Waziri Magufuli
alibainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Geita na Kagera wamefurahishwa
sana kuona kuwa hatimaye barabara hiyo muhimu inajengwa kwani hiyo ndiyo sehemu
pekee iliyokuwa imebaki ikiwa haina lami kwa barabara inayounganisha mikoa hiyo
ya ziwa.
No comments:
Post a Comment