Thursday, 18 April 2013

KUCHELEWA KWA MISHAHARA YA WALIMU WAPYA TATIZO SI SERIKALI

1
Waziri wa Utumishi, Mhe. Celina Ompeshi Kombani
Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.
Walimu wapya wanaochelewa kupata mishahara yao kwa wakati ni wale ambao kwa sababu zao wanakwepa kwenda kwenye vituo wanavyopangiwa na Wizara na kuripoti wanapotaka wao.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Utumishi, Mhe. Celina Ompeshi Kombani wakati akifafanua Bungeni suala la kuchelewa kwa mishahara ya Walimu shule za vijijini lililoulizwa na Mhe. Riziki Omar Juma (Viti Maalum).
Mhe. Kombani amesema baadhi ya walimu kwa makusudi huwa hawaendi kwenye shule wanazopangiwa na hivyo majina yao hayaonekani katika orodha ya shule wanazoamua kwenda ambapo mishahara yao hupelekwa katika vituo walivyopangiwa na hivyo walimu hujikuta wanachelewa kupata mishahara yao.

Katika jibu la msingi lililotolewa na Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa wa kuhusu swali hilo amesema kuwa serikali huwahudumia walimu wapya wanaoajiriwa bila kujali wamepangwa katika shule za vijijini au mjini ikiwemo kulipwa mishahara na staili zao nyingine.
Amesema mishahara kwa waajiriwa wote wapya hulipwa baada ya mwajiriwa kujaza fomu za ajira na kuwasilisha taarifa binafsi ikiwemo vyeti vya taaluma na kitaalamu.
Baada ya hatua hizo, Halmashauri husika huziingiza katika mfumo wa malipo ambao hupeleka moja kwa moja majina hayo kwa njia ya mtandao Ofisi ya Rais Menejementi ya Utumishi wa Umma, kwa ajili ya kuidhinishwa na maandalizi ya malipo ya mishahara kwa mwezi unaofuata.
 Amesema wanaochelewa kupata mishahara ni wale ambao majina yao huchelewa kutuma baada ya tarehe Nane ya mwezi.
Mhe. Majaliwa amesema mwalimu akichelewa kupata mshahara na yupo kituoni, Mkurugenzi wa Halmashauri anawajibika kumuhudumia ili aweze kujikimu.
 Amesema Serikali imekuwa ikituma fedha za posho katika Halmashauri kabla ya walimu kuripoti katika juhudi za kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi ikiwemo walimu.
Hata hivyo amekiri kuwepo na maeneo nchini ambayo mtandao hufanya kazi taratibu na hivyo husababisha baadhi ya walimu kutoingia katika orodha ya malipo kwa wakati na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha walimu wote ambao hawajaingizwa katika orodha wanahudumiwa ipasavyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...