Thursday, 18 April 2013

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) CHAKERWA NA SARAKASI BUNGENI

4
Chama Cha Mapinduzi kimekerwa na vurugu zinazoendelea katika vikao vya Bunge vinavyoondelea mjini Dodoma na kusisitiza kuwa kinachoendelea kwasasa ni dhihaka kubwa kwa wananchi na walipakodi ambao kimsingi ndio waliowatuma wabunge bungeni na ndio wanaowalipa.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara mjini Gairo akiwa katika ziara ya siku nane ya Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe we sekretari eti ya CCM jana, Katibu we Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema vurugu na ukaidi wa kanuni zinazoliongoza Bunge unaofanywa na wabunge wa Chadema zinathibitisha namna Chadema kilivyo chama cha wababaishaji.
Nape alisema tabia ya wabunge wa Chadema ya kutafuta umaarufu rahisi kwa kukiuka taratibu na kugomea kanuni halali zinazoendesha na kusimamia shughuli za Bunge haikubaliki.

“Wananchi waliwachagua kwenda Bungeni kuwasemea kero zinazowakabili, lakini wabunge hawa wa Chadema wamekuwa wakifanya kinyume chake, wamekuwa muda wote wakibisha na kukataa kila kitu zikiwemo kanuni zinazoliongoza Bunge, tukiacha hili liendelee litaharibu Bunge letu zuri, Jambo ambalo haikubaliki” alisisitiza Nape.
Aliongeza kuwa CCM inalaani kwa nguvu zote kile kilichotokea Bungeni Jana jioni, na kusisitiza kuwa kila Mtanzania kwa nafasi yake pia hana budi kukilaani kitendo hicho.
Juzi Wabunge watano wa Chadema walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana na vurugu za kukaidi amri halali ya Naibu Spika Job Ndugai, iliyomtaka Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kutoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki Mwigulu Nchemba.
Wabunge wengine waliofukuzwa baada ya kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Ndugai ni pamoja na Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...