Wednesday, 24 April 2013

MKAA WA MIFUPA YA NG’OMBE KUTUMIKA KUONDOA MADINI YA FLUORIDE KATIKA MAJI.

1
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Jumanne Maghembe (mbele)
Na Benedict Liwenga,  Dodoma.
SERIKALI imeandaa mkakati wa kusambaza teknolojia ya kutumia mkaa wa mifupa ya Ng’ombe kuondoa madini ya Fluoride katika maji ya kunywa na kupikia.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Jumanne Maghembe wakati akiwasilisha hotuba ya makadilio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2013/2014 mjini Dodoma leo.
 Amesema kwamba mkakati huo utaanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2013/14.
 Profesa Maghembe amesema kuwa kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuimarisha mbinu za usambazaji wa teknolojia katika Ukanda wa Bonde la Ufa na kutayarisha ramani inayoonyesha maeneo yenye kiwango kikubwa cha madini ya Fluoride katika maji. Ramani hiyo “itasaidia kuyatambua maeneo hayo wakati wa kuimarisha miradi ya Maji”.
Aidha, Profesa Maghembe amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yake itakarabati Maabara Kuu zote za mikoa pamoja na Ofisi ili kuweka mazingira mazuri ya kazi ya kukidhi matakwa ya kupata ithibati ambapo Tasmini huanzia kwenye majengo.
 Amesema pia maabara (za maji) zitaimarishwa na kujengewa uwezo kwa kununua ramani, vifaa vya maabara na madawa na watumishi kupatiwa mafunzo ili kuongeza ufanisi na tija katika usimamizi wa ubora wa maji.

 Mhe, Profesa Maghembe ameliomba Bunge kuidhinisha Wizara yake jumla ya shilingi 398,395,870,000 ili iweze kutimiza majukumu na malengo yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
 Amesema kati ya fedha hizo shilingi 18,952,654,000 ni Matumizi ya Kawaida na shilingi 379,443,220,000 ni Matumizi ya Maendeleo.
Katika fedha za Matumizi ya Kawaida shilingi 13,319,877,000 ni mishahara ya Watumishi na shilingi 5,632,777,000 ni fedha za Matumizi katika fedha za Maendeleo, shilingi 138,266,164,000 ni fedha za Ndani na shilingi 241,177,056,000 ni fedha za Nje.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...