Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai
(pichani) amewashangaa na kuwabeza wanaokejeli Serikali ya Awamu ya Nne
ya Uongozi wa Tanzania, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa
haijafanya lolote kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema
kuwa yeye binafsi ameshuhudia mazuri mengi na mafanikio mengi
yaliyoongozwa na Serikali ya Rais Kikwete kwa kuanzia kwenye eneo lake
mwenyewe.
Naibu
Spika Ndugai ameyasema hayo leo, Alhamisi, Aprili 11, 2013 wakati
alipopewa nafasi ya kuwasilimia wananchi kwenye Sherehe ya Uzinduzi wa
Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Miundombinu ya Kusambaza Umeme Mkoani
Dodoma na Wilaya ya Kiteto, Mkoa jirani wa Manyara chini ya Ufadhili wa
Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Millenium Challenge Corporation
(MCC).
MCC
imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 28.5 (sawa na dola 17.8) kwa ajili ya
ujenzi wa Mradi huo wa Kusambaza Umeme ikiwa ni sehemu ya msaada wa dola
za Marekani milioni 698 (sawa na Sh. trilioni 1.19) wa ujenzi wa miradi
mingi ya miundombinu katika Tanzania.
“Mheshimiwa
Rais, nianzie kwenye kijiji cha Mkoka ambako tulipo kwa sasa na nieleze
nini Serikali yako inakifanya kijiji hiki katika mwaka huu wa Bajeti
ili kuthibitisha jinsi Serikali yako chini ya uongozi wako inavyochapa
kazi,” amesema Naibu Spika Ndugai na kuongeza:
“Serikali
yako imekipa kijiji cha Mkoka sh. milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa
soko la kisasa na ujenzi huo unaendelea. Tunajenga machinjio ya kisasa
kwa gharama ya sh. milioni 40. Tunajenga mradi mkubwa wa maji kwa kiasi
cha sh. milioni 600 na shule zetu mbili tayari zimejengewa madarasa ya
nyongeza katika mwaka huu wa fedha,” amesema Ndugai na kuzidi kumwambia
Rais Kikwete:
“Siyo
hivyo tu. Serikali yako Mheshimiwa Rais imetuwezesha kupata fedha na
raslimali nyingine za kujenga ghala la mazao, kujenga maabara mpya
kwenye Sekondari yetu ya Kata na tumepatiwa kiasi cha sh. milioni 700
kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbili ambazo zote zitaishia kwenye Soko
la Kimataifa la Mahindi la Kibaigwa, ujenzi ambao utawezesha wakulima
kufikisha mahindi yao kwenye soko hilo kwa urahisi kuliko ilivyo sasa.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
12 Aprili, 2013
No comments:
Post a Comment