Afisa
Ubalozi wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bw. Justin
Kisoka ambaye pia alikuwa Mratibu wa Kamati ya Tano inayohusika na
masuala ya Utawala na Bajeti akiwasilisha siku ya Ijumaa, taarifa ya
Kamati hiyo mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo
ilihusisha maazimio Nane ambayo Baraza Kuu liliyapisha kwa kauli moja,
likiwamo lile linaloidhinisha ujenzi wa Majengo ya Taasisi ya Kimataifa
ya Kumalizia Mashauri ya Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ( ICTR) Tawi la Arusha. Majengo hayo ya kisasa
yatajengwa katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha.
*********
Na Mwandishi Maalum
Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja Azimio
linalopendekeza kuidhinishwa kwa hatua zote za Ujenzi wa Mradi wa
Taasisi mpya ya Kimataifa itakayochukua majukumu ya Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR).
Mradi huo
wa majengo ya kisasa, utajengwa katika eneo la LakiLaki Jijini
Arusha-Tanzania na utahusisha Ofisi, vyumba vya mahakama, na sehemu
ya kutunzia nyaraka na kumbukumbu zote za ICTR. Eneo hilo la Laki Laki
limetolewa na Serikali ya Tanzania kwa Umoja wa Mataifa.
Baraza
Kuu limepitisha Azimio hilo katika mkutano wake uliofanyika siku ya
Ijumaa ( April 12),mkutano ambao pia, Baraza lilipokea na kupitisha
maazimio mengine Nane yaliyowasilishwa na Kamati ya Tano inayohusika
na masuala ya Utawala na Bajeti katika Umoja wa Mataifa.
Taasisi
hiyo mpya ijukulikanayo kama Mfumo wa Kimataifa wa Kumalizia Mashauri
Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari au kwa
kimombo ( International Residual Mechanism for Criminal Tribunal )-
Tawi la Arusha pamoja na kuhifadhi nyaraka itasimamia kesi za Masalia
ambazo zitakuwa bado hazijakamilia baada ya ICTR kumaliza muda wake
mwakani.
Azimio
hilo pamoja na mambo mengine, linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
kuweka bayana uwajibikaji na uangalizi wa kina katika ujenzi wa mradi
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria, taratibu, kanuni na
miongozo yote ya Umoja wa Mataifa inayohusu manunuzi/ugavi
inafuatwa ipasavyo katika utekelezaji wa mradi huu.
Gharama
za mradi zinatarajiwa kuwa kiasi cha dola za kimarekani 8.78 Milioni (
takribani Sh.14 Bilioni). Fedha hizi zinalipwa na Nchi wanachama wa
Umoja wa Mataifa. Mradi unatarajiwa kukamilika kabla ya mwishoni mwa
mwaka 2015.
Aidha
kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu pia limeishukuru Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea na jukumu la kufuatilia kwa
karibu mchakato wote unaohusiana na utekelezaji wa mradi na vilevile
katika kuhakikisha kwamba inashirikiana na Umoja wa Mataifa
kufanikisha Mradi huu.
Halikadharika
kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu limeelezea kufurahishwa na
maendeleo ya utekelezaji wa mradi hasa kwa kutumia ujuzi wa ndani,
(Local knowledge) katika ubunifu wa majengo (design), upatikanaji wa
meneja wa mradi na maandalizi ya kina ya gharama za ujenzi.
Pamoja na
pendekezo la kuidhinishwa kwa hatua za ujenzi wa mradi , Baraza pia
kupitia Azimio hilo , linamtaka KatibuMkuu kufanya juhudi zote
zitakazo pelekea kupunguza muda wa ujenzi wa mradi .
Katika
hatua nyingine, Baraza Kuu pia linamtaka Katibu Mkuu kuanza
mazungumzo na Asasi nyingine za Kimataifa ikiwamo ile ya Mahakama Afrika
itakayoshughulikia Haki za Binadamu, juu ya namna bora ya
kushirikiana katika matumizi ya miundo mbinu hiyo katika siku za usoni.
Mwaka
2010 Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio
nambari 1966 la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia Mashauri ya
Masalia kwa zilizokuwa Mahakama za Kimataifa za Mauaji ya Kimbari
yaliyotokea nchini Rwanda ( ICTR) na Mauaji ya halaiki yaliyotokea
katika iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani ( ICTY).
Katika
azimio hilo Baraza Kuu la Usalama lilibainisha wazi kwamba Arusha
ndiyo itakuwa makao ya Tawi la mfuno huo mpya na The Hague ikiwa ni
makao ya Tawi jingine.
No comments:
Post a Comment