Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt.Emmanuel Nchimbi.
Mahmoud Ahmad Arusha
Serikali imesema kuwa Tukio la ulipuaji wa bomu la kutupwa kwa mkono kwenye mkutano wa kampeni wa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) halikubaliki na sio la kibinadamu ambalo linaashiria kuvuruga amani.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt.Emmanuel Nchimbi wakati alipotembelea na kujionea eneo la tukio la wahanga wa tukio hilo la bomu katika hospitali za Seliani pamoja na hospitali ya mkoa ya Mounti Meru zilizopo jijini Arusha.
Nchimbi amebainisha kuwa hadi sasa jumla ya watu waliojeruliwa katika tukio hilo ni 70 ambapo kati yao wawili wamepoteza maisha na wengi wawili wapo mahututi katika hospitali ya Seliani wanapoendelea na matibabu huku wengine nane wakiwa wameruhusiwa kurudi majumbani.
Amesema kuwa wao kama serikali wamepokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa na tukio hilo halikubaliki na sio la kibinadamu na lina nia mbaya ya kuvuruga amani na wao kama serikali wanalilaani kwa nguvu zote.
“Kitendo cha kutupwa kwa bomu Serikali inakilaani na kuwa kitendo hichi kinalaaniwa kwa nguvu zote anawataka wananchi kuwa watulivu wakati huu na kuimarisha usalama na kuwa watoe taarifa pale mtakapohisi matukio kama haya”amesema Nchimbi.
Aidha amesema kuwa jeshi la polisi limetuma wapelelezi wa mabomu kuja na kuwa upelelezi huo utasimamiwa na mkuu wa operesheni wa jeshi hilo Paul Chagonja huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola huku upelelezi wa awali ukionyesha kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono.

No comments:
Post a Comment