1.0 UTANGULIZI
Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana tarehe 15 hadi 26 Oktoba 2013 kutekeleza Majukumu yake , Jijini Dar es Salaam kabla ya Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 29 Oktoba hadi 08 Novemba, 2013. Kwa kawaida, wiki mbili kabla ya Mkutano wa Bunge, Kamati za Kudumu za Bunge hukutana ama Dar es Salaam, Dodoma au Zanzibar kwa mujibu wa Kanuni ya 117(4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la April 2003.
Kutokana na kuanza kwa Kamati hizi, Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili jijini Dar es Salaam ifikapo jumapili tarehe 13 Oktoba 2013 tayari kwa kuanza vikao siku ya tarehe 15 Oktoba, 2013 baada ya Siku Kuu ya Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere.
2.0 SHUGHULI ZITAKAZOTEKELEZWA
2.1 Kamati zitafanya Uchambuzi wa Miswada ya Sheria ambapo Miswada Mitatu inatarajiwa kuchambuliwa ikiwa ni pamoja na kupokea maoni ya wadau kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali No 3. Wa Mwaka 2013 utakaoshughulikiwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
2.2 Aidha, Kamati za Usimamizi wa Fedha za umma zitapitia Hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka 2011/2012.
2.3 Kamati kumi na moja za sekta pamoja na majukumu mengine, zitapokea na kujadili Taarifa mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi za Umma
3.0 ZIARA ZA KAMATI
3.1 Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) itafanya ziara ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kwenye Halmashauri za Wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro.
Kamati nyingine tano za sekta; Ardhi, Maliasili na Mazingira; Miundombinu; Huduma za Jamii; Kilimo, Mifugo na Maji; na Kamati ya Ulinzi na Usalama zitafanya ziara fupi na ndefu ndani na Nje ya Dar es Salaam kwa madhumuni ya kufuatilia utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali na Taasisi zake.
Ratiba zote za Kamati zinapatikana kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge
Dar es Salaam
13 Oktoba 2013
No comments:
Post a Comment