Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewapongeza wanahabari ,wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari
nchini kwa kuadhimisha Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani (World Press Freedom Day)
leo, Ijumaa, Mei 3, akiwahakikishia kuwa Serikali yake itaendelea
kukuza, kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari ulioshamiri kwa
kiwango cha juu kabisa nchini kwa sasa.
Aidha, Rais
Kikwete amesisitiza kuwa Serikali yake na yeye binafsi, kama mdau wa
habari, wataendeleza kuelekeza nguvu kubwa katika kupanua Uhuru wa
Habari kwa sababu uhuru huo ni kigezo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi
na kijamii ya Tanzania na katika kujenga na kupanua demokrasia nchini.
Katika
salamu zake kwa wanahabari, wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari
nchini ambayo inasherehekea Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Dunia
kitaifa mjini Arusha leo katika shughuli zilizoandaliwa na Taasisi ya
Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Tawi la Tanzania, Rais Kikwete amesema:
“Kama
muumini na mdau wa Uhuru wa Habari ambao ni sehemu ya Uhuru Mpana Zaidi
wa Kutoa Maoni (Freedom of Expression), napenda kuwapongezeni
wanahabari wote nchini na wadau wenzenu duniani katika kusherehekea siku
hii ya kuadhimisha Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ambayo
kitaifa hapa kwetu inaadhimishwa na shughuli zilizoandaliwa na MISA-Tan
mjini Arusha.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais: “Sisi
katika Tanzania tunayo kila sababu ya kusheherekea Siku hii ya leo ya
Uhuru wa Habari nchini kwa sababu sote ni wadau wa habari ni mashahidi
wa mafanikio makubwa na mengi katika nyanja ya habari katika miaka 20
iliyopita katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, naungana nanyi katika
kusheherekea na kuadhimisha mafanikio haya makubwa.”
Siku ya
Uhuru wa Habari Duniani ambayo chimbuko lake ni Mkutano wa Waandishi wa
Habari wa Afrika waliokutana na kutoa Tamko la Windhoek (Namibia) – the Windhoek Declaration on Promoting an Independent and Pluralistic African Press pamoja na kuanzisha Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika – Media institute of Southern Africa (MISA), Mei 3, mwaka 1991, ilichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya Uhuru Duniani mwaka 1993.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Napenda
kutumia Siku hii ya leo kuwapongezeni tena kwa kazi yenu nzuri ambayo
imeendelea kuchangia maendeleo ya nchi yetu kupitia njia ya kuhabarisha,
kuelimisha na kuburudisha wananchi. Vile vile, napenda kutumia nafasi
ya Siku ya leo kuwaelezeeni utayari wa Serikali yetu kuendelea
kuithamini kazi hii nzuri. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuifanya
kazi yenu kwa kuongozwa na misingi mikuu ya weledi wa taaluma ya
uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha,
kama ambavyo tumekuwa tukifanya, napenda kuwahakikishieni kuwa mimi
binafsi na Serikali ninayoingoza nitaendelea kushirikiana nanyi katika
kupanua, kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari nchini ikiwa ni haki
ya waandishi kufanya kazi yao kwa mazingira mwafaka ya kisiasa,
kiuchumi, kisheria na kijamii. Vile vile, napenda kuwahakikisheni
tutaendelea kushirikiana nanyi katika kulinda uhuru wa wapata habari
nchini ambao ni muhimu kama ulivyo uhuru wa vyombo vya habari.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
03 Mei, 2013

No comments:
Post a Comment