Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (kulia) na Makamu
wake Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani katika moja ya mikutano na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. (Picha na Tume ya Katiba).
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya mwongozo wa uundwaji wa Mabaraza
ya Katiba yatakayoundwa na kuendeshwa na taasisi, asasi, vyama na
makundi ili kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Katiba
itakayoandaliwa na Tume.
Kwa
mujibu wa rasimu ya mwongozo iliyotolewa na Tume leo (Jumatatu, Mei 10,
2013) na kusambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo tovuti
(www.katiba.go.tz) na ukiwemo ukurasa wa facebook wa Tume hiyo (Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Tanzania), mwisho wa wananchi na wadau mbalimbali
kuwasilisha maoni yao kuhusu mwongozo huo ni Mei 19 mwka huu (2013).Rasimu
hiyo inafafanua kuwa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na
makundi hayo unapaswa kutegemea katiba, kanuni, randama au 'charter' ya
asasi husika.
"Miongoni
mwa asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana
yanayoweza kuunda Mabaraza ya Katiba ni kama jumuiya ya kidini, chama
cha siasa, asasi ya kiraia, taasisi ya elimu ya juu, chama cha
wanahabari," inasomeka rasimu hiyo ya Tume itakayochapishwa katika
magazeti ya Habari Leo, Zanzibar Leo na Mwananchi ya kesho (Jumamosi,
Mei 11, 2013) na kurudiwa katika magazeti hayo Jumatatu (Mei 13, 2013).
Kwa
mujibu wa Tume, asasi nyingine zinazoweza kuunda mabaraza hayo ni
Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Wakulima,
Chama cha Wafugaji, Baraza la Watoto, Taasisi ya Wafanyabiashara, Baraza
la Wanawake, Taasisi ya Wanataaluma, Baraza la Vijana, Baraza la Wazee
na Kundi au makundi ya watu wenye malengo yanayofanana au yale yenye
mahitaji maalum katika jamii.
Katika
rasimu hiyo, Tume inapendekeza asasi zinazotarajia kuunda mabaraza kutoa
taarifa ya maandishi kwa Tume kuhusu kusudio la kuunda, kuendesha na
kusimamia mabaraza ya katiba.
"Taarifa
hiyo itawasilishwa katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba moja kwa
moja Makao Makuu, mtaa wa Ohio, Dar es Salaam au ofisi ndogo Zanzibar
au kutumia posta (S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P. 2775, Zanzibar)
au barua pepe ( katibu@katiba.go.tz)," inasomeka sehemu ya rasimu hiyo.
Mabaraza
ya Katiba yanaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa mujibu wa kifungu cha 18(6) cha
sheria hiyo, Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu
wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa
wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na kisha
kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment